Penzi Bila Maumivu (Sehemu ya 1)

Simulizi: PENZI BILA MAUMIVU

Mtunzi: NYEMO CHILONGANI

SEHEMU YA KWANZA

“Sijui atazaliwa mtoto gani.”
“Labda wa kiume.”
“Mh! Mimi napenda awe mtoto wa kike ili na sisi tujivunie kwa mara nyingine.”
“Ila yeye mwenyewe si alitaka wa kiume?”
“Nani?”
“Sangiwa!”
“Ndivyo alivyosema?”
“Ndivyo nilivyosikia, eti kwa sababu ana watoto wengi wa kike, hivyo anataka apate na mwingine wa kiume!”
“Mh! Nafikiri hizo ni tetesi tu.”
Yalikuwa ni mazungumzo ya wanawake wawili miongoni mwa watu wengi waliokuwa wamekusanyika nje ya nyumba pekee iliyokuwa imeezekwa bati na kujengwa kwa matofali, nyumba ya mzee aliyeaminika kuwa na fedha nyingi katika Kijiji cha Chibe kilichokuwa mkoani Shinyanga.
Kila mtu alitaka kujua ni mtoto gani ambaye angezaliwa na mke wa Sangiwa aliyekuwa na pesa nyingi kijijini hapo. Watu walimpenda Sangiwa kwa kuwa hakuwa mtu wa majivuno, kile alichokuwanacho, alitamani wengine pia wakipate.

Kipindi cha nyuma alikuwa na maisha magumu, masikini kama watu wengine, alidharaulika sana kijiji hapo, hakuwa na nyumba kwani wazazi wake walipofariki, hata ile nyumba aliyokuwa akiishi, akafukuzwa.
Alipitia maisha magumu, hakuona afadhali ya maisha hata siku moja, kila siku alikuwa mtu wa kuomba misaada tu, wapo waliokuwa wakimsaidia lakini pia kulikuwepo na wale waliokuwa wakimnyima.

Alipoona kijijini Chibe maisha yalikuwa magumu, hapo ndipo alipoamua kuhama na kuhamia kijiji cha jirani cha Beda. Maisha hayakubadilika, bado aliendelea kuishi kwenye maisha ya kimasikini hali iliyomfanya kwenda kuomba kazi kwa mzee Mwiku aliyekuwa kijijini hapo.
Kwa kuwa mzee huyo alikuwa na ng’ombe wengi, akampa Sangiwa kazi ya kuwa mchungaji wa mifugo yake. Hilo halikuwa tatizo kwa Sangiwa, kwa kuwa alikuwa na shida, hakuwa na pesa, akakubaliana naye na hivyo kuanza kazi hiyo.

Ilikuwa kazi ngumu mno, kitendo cha kuchunga zaidi ya ng’ombe elfu kumi huku akiwa na wenzake wawili tu ilikuwa kazi kubwa. Kuna kipindi wanyama hao walikuwa wakiingia katika mashamba ya watu, waliwafukuza na hata wakati mwingine kusemwa sana huku wakipokea vitisho vya kila aina.
Waliogopa lakini hawakuwa na jinsi, hawakuachana na kazi hiyo, waliendelea kuchunga kila siku. Walipokuwa wakirudi na kufika nyumbani, walitengewa maziwa, ugali na kunywa.
Hayo ndiyo maisha waliyokuwa wakiishi, walikubaliana nayo kwa kuwa hawakuwa na lolote la kuweza kufanya. Urafiki wake na wachungaji wenzake, Milenze na Olembetu ukazidi kukua kwa kuwa kila wakati walikuwa pamoja.

“Umemuona Frida?” aliuliza Milenze.
“Frida gani?”
“Mtoto wa bosi.”
“Amefanya nini?”
“Alivyokuwa akikuangalia!”
“Mimi?”
“Ndiyo! Alikuwa akikuangalia sana, mpaka nikashangaa.”
“Haiwezekani, hawezi kuniangalia hivyo, au kama nilikosea kuvaa hii suruali,” alisema Sangiwa.
“Mh! Sidhani. Ila nahisi kuna kitu.”
“Kitu gani?”
“Au anakupenda!”
“Anipende mimi masikini?”
“Hata mimi nashangaa!”

Hapakuwa na mtu aliyejiamini, kila mmoja alijiona kuwa masikini hivyo kupenda na msichana aliyetoka katika familia ya mtu mwenye pesa lilionekana kuwa tatizo. Siku hiyo, Sangiwa akaamua kufuatilia kujua kama kile alichoambiwa kilikuwa kweli au la.
Walipofika nyumbani, wakatengewa chakula na wasichana wa mzee Mwiku akiwemo huyo Frida. Kama alivyoambiwa ndicho kilichotokea, muda mwingi Frida alikuwa akimwangalia mpaka kumfanya kijana huyo kuanza kuogopa.
Alikuwa masikini sana, alikuja kijijini hapo akiwa peke yake, hakuwa na kitu chochote kile zaidi ya zile nguo alizokuwa amezivaa. Alikaribishwa kijijini hapo na mwisho wa siku kupewa kazi na mzee huyo.

Hakutaka kuamini kile kilichokuwa kikiendelea, eti msichana ambaye baba yake alikuwa tajiri ampende yeye masikini asiyekuwa na kitu, kwake ulionekana kuwa muujiza mkubwa.
Sangiwa hakutaka kukubaliana na uhalisia uliokuwepo kwamba alipendwa na msichana huyo, alichokifanya ni kuachana naye na kuendelea na maisha yake kama kawaida.

Frida hakupunguza kumwangalia Sangiwa, kila alipokuwa akikaa, macho yake yalikuwa usoni kwa kijana huyo, alitokea kumpenda mno, moyo wake ukatekwa na hapakuwa na njia nyingine ya kufanya zaidi ya kupanga kumwambia ukweli.
“Hivi atanikubalia kweli?” alijiuliza.
“Sidhani, lakini mbona kama ananiogopa? Mungu! Naomba anikubalie nitakapomwambia ukweli,” alisema Frida huku mapigo yake ya moyo yakidunda mno.

Hakuwa na jinsi, hakutaka kuendelea kuteseka, alitaka kuhakikisha mvulana huyo anakuwa wake peke yake. Alitumia muda mwingi sana kujipanga ili pindi atakaporudi basi aweze kumwambia ukweli juu ya kilichokuwa kikiendelea moyoni mwake.
Ilipofika saa 12 jioni, kwa mbali akaona ng’ombe na wanyama wengine wakianza kurudishwa, hakuwa na wasiwasi kwamba hiyo ilikuwa mifugo yao na miongoni mwa wachungaji wale alikuwepo mvulana aliyekuwa akimpenda sana.

Walipofika, Frida akaanza kupitisha macho yake kuwaangalia wachungaji wale, kitu kilichoonekana kumshtua sana, Sangiwa hakuwepo.
“Mh! Sangiwa yupo wapi?” alijiuliza pasipo kupata jibu lolote lile.
Moyo wake ukajawa na presha kubwa, kitendo cha kutokumuona kijana huyo akirudi na wachungaji wale kilimshtua kwa kuona inawezekana kulikuwa na tatizo, au alikimbia kwani vijana wengi kwa kipindi hicho walikuwa wakitoroka sana kuelekea mjini kutafuta maisha.

Hakutaka kukubali, hakujisikia amani moyoni mwake, kwani hata alipoangalia kwa mbali katika njia ile waliyokuwa wakiitumia wachungaji, hakuweza kumuona Sangiwa.
“Naomba nikuulize kitu Olembetu,” alisema Frida, aliamua kumfuata mmoja wa wachungaji wale.
“Kitu gani?”
“Sangiwa yupo wapi?” aliuliza Frida.
“Kuna tatizo lilitokea.”
“Tatizo gani?”
“Kwanza baba yupo?”
“Ndiyo! Yupo.”
“Ngoja nikamuone,” alisema Olembetu.
“Kwanza niambie nini kimetokea,” alisema Frida huku akimvuta Olembetu.
“Nitakuja kukwambia, subiri kwanza,” alisema Olembetu na kuondoka mahali hapo.
Frida akawa na hofu moyoni mwake, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, aliambiwa kulikuwa na tatizo lililokuwa limetokea lakini kila alipotaka kufahamu tatizo hilo lilikuwa lipi, akakosa jibu.

Akabaki akiwa na presha kubwa, akabaki mlangoni huku akionekana kuwa na mawazo. Hakuwa na hamu ya kula wala hamu ya kufanya jambo lolote lile, akili yake yote ilikuwa ikimfikiria Sangiwa tu.
Wala hazikupita dakika nyingi, mlango ukafunguliwa, baba yake, mzee Mwiku akatoka huku akiwa na hasira kubwa, alichokifanya mzee huyo, akachukua viatu vyake vilivyokuwa mlangoni na kuondoka mahali hapo huku akionekana kama mtu aliyechanganyikiwa.
Hali hiyo ikamtia hofu Frida.

Inaendelea….


Asante kwa muda wako kusoma kwenye blog hii, natumaini umefarijika vya kutosha. Tutuunga mkono ili tuendelee kuweka simulizi hizi kila siku unaweza kutununulia kikombe cha kahawa kama mchango wako kuanzia Tsh 1000 au zaidi kupitia Airtel Money – 0686638386 – MUSA MWAKISASA

What do you think?

954 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Harmonize ft Awilo Longomba & H baba – Attitude (Music + Lyrics)

MaxCoach 2.3.2 – Online Courses & Education WP Theme