Penzi Bila Maumivu (Sehemu ya 2)

Simulizi: PENZI BILA MAUMIVU

Mtunzi: NYEMO CHILONGANI

SEHEMU YA PILI

Wachungaji walikuwa kwenye wakati mgumu, walijitahidi kuwazuia ng’ombe wao kwenda katika mashamba ya watu wengine lakini hali hiyo ilikuwa ngumu kwao.
Ng’ombe walikimbilia kwenye mashamba ya watu yaliyokuwa na mavuno mengi na kuanza kula mahindi. Sangiwa, Olembetu na Milenze waliendelea kujitahidi kuwazuia ng’ombe wale lakini ilishindikana kabisa.
Waliwafahamu vizuri wakulima, mara kwa mara walikuwa wakipambana nao na hata wakati mwingine kuuana kwa kile kinachosemekana kuwa dharau kutoka kwa wafugaji ambao walionekana kuwaachia ng’ombe wao makusudi na kwenda kuvamia mashamba yao.
Kwa kila ng’ombe aliyekuwa akiingia shambani mwao, walikuwa wakiwakamata, wanawachinja na maisha kuendelea.

Wakati Sangiwa na wenzake waliposhindwa kuwazuia ng’ombe wale na kuingia mashambani, tayari wakajua ugomvi mkubwa ungetokea kwani mara kwa mara tukio kama hilo linapotokea, wakulima hupandwa na hasira na kuwaua ng’ombe au hata kuwachukua wachungaji wenyewe.
Wote walionekana kuwa na hofu, kitendo cha ng’ombe wale kuingia katika shamba la mzee Matumbo tayari kukaonekana kuwa na ugomvi mzito ambao ungetokea. Vijana wa mzee huyo ambao mara kwa mara walikuwa shambani mule wakilima au hata kuhakikisha mazao yanachungwa, walipowaona ng’ombe wale, wakawakamata.

“Jamani tunaomba mtusamehe,” alisema Sangiwa, alionekana kutia huruma, kosa kubwa la kutokuweza kuwazuia ng’ombe wale kuingia shambani mule, tayari kukaonekana kama kungetokea ugomvi mkubwa.
“Kwa nini mmewaruhusu ng’ombe kuingia shambani kwetu?” aliuliza kijana mmoja, alionekana kuwa na hasira tele.
“Hatukuwaruhusu, tulishindwa kuwazuia,” alijibu Sangiwa huku akionekana kuwa na hofu.
“Tunawaua kama kawaida yetu.”
“Naomba msiwaue, nawaombeni tafadhali,” alisema Olembetu huku akipiga magoti.

Wakati maongezi yakiendelea mahali hapo, ghafla mzee Matumbo akatokea mahali hapo, alipowaona ng’ombe wale shambani kwake, akashikwa na hasira, akaanza kuwasogelea wachungaji wale huku akionekana kuwa na shari kabisa.
“Kwa nini mmewaruhusu ng’ombe wetu kuingia shambani kwangu?” aliuliza huku akionekana kughadhibika.
“Hatukuwaruhsu mzee, naomba utusamehe, walituzidi nguvu,” alisema Sangiwa.
“Ng’ombe wa nani hawa?”
“Mzee Mwiku.”
“Kamuiteni mwenyewe, la sivyo ng’ombe hawatoki hapa,” alisema mzee yule.
“Mzee, tunakuomba utusamehe.”
“Nimesema kamuiteni, kama hamtaki, mmoja wenu abaki na ng’ombe waende,” alisema mzee huyo kwa sauti ya juu iliyokuwa na hasira.
“Hakuna tatizo. Acha nibaki mimi,” alisema Sangiwa maneno yaliyoonekana kuwashangaza wenzake wote.

Hapakuwa na cha kufanya, alitaka mwenyewe kubaki ilimradi wale ng’ombe wachukuliwe na kurudishwa nyumbani. Kwa mzee Matumbo, hakutaka kufanya kitu chochote kibaya, alimheshimu mzee Mwiku kwa kuwa walifahamiana sana.
Alikuwa mzee tajiri aliyekuwa na mifugo mingi, alipendwa na watu wengi, si katika kijiji chake bali hata watu wa vijiji vingine walimpenda mzee huyo aliyeonakana kuwa na roho ya huruma na kusaidia watu.
Kutaka kijana mmoja abaki, kwake ilikuwa kama nafasi ya upendeleo, hakutaka kuingia kwenye ugomvi na mzee huyo kwani kama jambo hilo lingetokea, mapigano yake yangekuwa makubwa na kusingeweza kupatikana kwa amani milele.
Wakati huo mzee Mwiku alikuwa njiani, alichanganyikiwa, alipoambiwa kijana aliyekuwa akimpenda kuliko wote, Sangiwa alizuiwa na mzee Matumbo kulimuumiza na hivyo akaamua kwenda huko yeye mwenyewe.

Mwendo wake ulikuwa ni wa harakaharaka, hakutaka kuangalia nyuma, wakati mwingine alikuwa akikimbia kwa kuona alikuwa akichelewa.
Binti yake, Frida hakutaka kubaki nyumbani, hakutaka kuona mvulana aliyekuwa akimpenda sana, Sangiwa akamatwe sehemu halafu yeye awe na amani nyumbani, alipomuona baba yake akiondoka, naye akaanza kumfuata kwa nyuma, ila alikuwa mbali.
Kila alipopiga hatua kadhaa, alikuwa akijificha, hakutaka kuonekana kabisa. Safari iliendelea, baada ya mwendo wa dakika arobaini na tano, wakaanza kuingia katika sehemu kubwa iliyoonekana kuwa kama shamba kubwa, huko ndipo mzee Mwiku alipokutana na mzee Matumbo.
“Afadhali umekuja,” alisema mzee Matumbo.
“Kuna tatizo?”
“Ndiyo lipo. Unamfahamu huyu?” aliuliza mzee Matumbo.
“Ndiyo namfahamu, ni kijana wangu.”
“Sawa. Ng’ombe wako walirudi tena shambani kwangu,” alisema mzee Matumbo, tayari kigiza kikaanza kuingia.
“Naomba umruhusu aondoke, sisi tubaki tukizungumza kama wazee,” alisema mzee Mwiku, hilo halikuwa tatizo, Sangiwa akaruhusiwa kuondoka.

Njiani hakutaka kutembea, mwendo wake ulikuwa ni kukimbia tu, alitaka kuwahi nyumbani kwani giza lile lililokuwa likikaribia kuingia, lilimuogopesha sana. Alikimbia mpaka alipotoka nje ya mashamba yale, hakutaka kuangalia nyuma, macho yake yalikuwa mbele tu.
Moyoni alimshukuru Mungu, hakuamini kile kilichotokea, kitendo cha kuruhiswa kuondoka huku akijua kulikuwa na ugomvi mkubwa baina ya wakulima na wafugaji, kwake aliona kama muujiza.
“Sangiwaaaa…..” ilisikika sauti nyuma yake.
Kwanza akaogopa, tayari giza lilibakia dakika chache kukamilika, alipoisikia sauti hiyo, akaogopa, alijua alikuwa porini, sasa ni nani aliyekuwa akimuita? Hofu ya kudhani sauti hiyo ilikuwa ni ya jini au mchawi ikamuingia, hivyo akaongeza kasi.
“Sangiwa nisubiri….Sangiwa nisubiri…” ilisikika sauti ile.
Masikioni mwake haikuwa ngeni, aliifahamu vilivyo, ilikuwa ni sauti ya msichana Frida, lakini pamoja na hayo, hakutaka kusimama.

Aliendelea kukimbia mpaka alipofika umbali fulani, sauti ile iliendelea kumuita, akaona bora asimame, kama ilikuwa ni ya jini kama alivyofikiria, hakuwa na jinsi, alikuwa tayari kufa.
Akageuka nyuma, kwa mbali akaanza kumuona mtu akija kwa kasi, mwili wake ukazidi kutetemeka, mapigo ya moyo yakazidi kumdunda kwa kasi kwa kuona kulikuwa na hatari iliyokuwa ikimsogelea mbele yake.
Akakosa nguvu za kukimbia, kikafika kipindi akajuta kwa nini alisimama kumsubiria mtu huyo aliyekuwa akija kwa kasi, alipokaribia, akamwangalia, alikuwa msichana aliyevalia gauni refu, alipokaribia zaidi, akagundua kwamba alikuwa Frida.
“We Frida, unafanya nini huku porini?” aliuliza Sangiwa huku akionekana kushangaa.
“Nimekufuata wewe.”
“Umenifuata mimi?”
“Ndiyo! Niliambiwa kwamba upo huku. Nini kilitokea?”
“Hapana, hebu twende nyumbani.”
“Subiri kwanza. Niambie,” alisema Frida.

Kadiri walivyokuwa wakiongea na ndivyo msichana huyo alivyozidi kumsogelea Sangiwa mpaka kumfikia karibu kabisa kama watu waliotaka kukumbatiana. Mapigo ya moyo wa Sangiwa yakazidi kudunda, akazidi kuingiwa na hofu, kuwa na binti wa mzee Mwiku porini, tena usiku, kulimtia hofu.
“Frida…” aliita Sangiwa wakati msichana huyo akishika maeneo ya zipu.
“Nakupenda. Naomba unipe.”
“Unasemaje?”
“Naomba unipe,” alisema Frida.
Hata kabla Sangiwa hajasema chochote, ghafla wakaanza kuzisikia sauti za watu wakija kule walipokuwa, zilikuwa kama sauti za watu watatu, walipozisikiliza vizuri, waliigundua sauti ya mtu mmoja, alikuwa mzee Mwiku.
Kila mmoja akaogopa.
“Baba…” alisema Frida huku akionekana kutetemeka.

Akili ya Sangiwa ikacheza fasta, aliona kama asingeweza kufanya kitu cha ziada basi wangeonekana mahali hapo jambo ambalo lingekuwa baya sana kwake, alichokifanya, tena kwa haraka sana ni kumshika mkono Frida na kumpeleka katika kichaka kilichokuwa pembeni.
“Nyamaza, usipige kelele,” alisema Sangiwa kwa sauti ya chini na Frida kutii.
Walikaa pale mpaka walipomuona mzee Mwiku akipita na watu wengine wawili, alikuwa mzee Matumbo na kijana mwingine, walikuwa wakimsindikiza kuelekea Beda.
Waliendelea kubaki kichakani pale mpaka walipopita na ndipo wakatoka na kusimama huku wakiangalia kule wazee wale walipoelekea.
“Si unaona ulitaka kusababisha tukamatwe,” alisema Sangiwa.
“Naomba unisamehe, lakini ninakupenda Sangiwa,” alisema Frida kwa sauti ya chini.
Sangiwa hakutaka kuelewa kitu chochote, alichomwambia ni kwamba walitakiwa kuondoka mahali hapo na kurudi kijijini tena kwa kupitia njia nyingine tofauti na ile waliyopita wazee wale.

Hiyo ndiyo ilikuwa siku ya kwanza kwa Frida kumwambia Sangiwa alikuwa akimpenda. Kwa kijana huyo, mambo yalionekana kuwa magumu, hakutaka kuwa na msichana huyo kwa kuwa alifahamu mapenzi hayakuwa na siri, hivyo kuna siku baba yake angegundua hilo.
Kwa Frida, maisha yalikuwa magumu, hakutaka kuelewa chochote kile, kila siku ilikuwa ni lazima kutafuta muda maalumu na kuzungumza na Sangiwa. Alimuonyeshea dalili zote kwamba alikuwa akimpenda, hakuona kama kulikuwa na umuhimu wa kuficha chochote kile.
Siku zikakatika, Frida, ambaye alipewa jina hilo kama mrithi wa Mzungu aliyewahi kuja mahali hapo, akaendelea kukua zaidi, maungo yake yakatanuka na kifua chake kujaa kitu kilichomuweka

Sangiwa kwenye wakati mgumu.
“Leo nahitaji,” alisema Frida huku akionekana kumaanisha kile alichokisema. Ilikuwa imepita miaka miwili, katika kipindi chote hicho alikuwa akizungushwa tu.
“Haiwezekani.”
“Kwa nini isiwezekane? Mimi si ni mpenzi wako?”
“Ndiyo! Lakini haiwezekani,” alisema Sangiwa huku akionekana kuogopa.
“Hapana, leo utanipa tu, ukikataa namwambia baba ulitaka kunibaka,” alisema Frida.
Maneno hayo aliyozungumza yalikuwa mwiba mkali moyoni mwa Sangiwa, hakuonekana kutania hata kidogo, alimaanisha kile alichokizungumza kwamba endapo asingekubali kufanya naye mapenzi basi ilikuwa ni lazima kumwambia baba yake alitaka kumbaka.
Kwa Sangiwa ukawa mtihani mgumu, hakutaka binti huyo akamwambie baba yake, alichokifanya, tena kishingo upande ni kukubaliana naye tu na mchezo kufanyika.

Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kila kitu, wakazidi kupendana kila siku mpaka kikafika kipindi ambacho Sangiwa akaacha mzee Mwiku ajue, na mambo yalipogundulika, Sangiwa akaamua kumuoa msichana huyo na kupewa ng’ombe themanini kama zawadi ya kuanza maisha yake.
Haohao ng’ombe ndiyo waliobadilisha maisha yao, Sangiwa alikuwa na akili ya maisha, kupitia ng’ombe hao, waliongezeka, akaanza kuwakamua maziwa na kwenda kuyauza mjini Shinyanga.
Ilikuwa biashara kubwa na yenye wateja wengi ambapo kidogokidogo akaanza kufanikiwa. Maisha yake yakabadilika na mpaka mwaka mmoja ulipopita, mkewe akajifungua mtoto wake wa kwanza wa kiume aliyempa jina la Malima.

Inaendelea…


Asante kwa muda wako kusoma kwenye blog hii, natumaini umefarijika vya kutosha. Kutuunga mkono ili tuendelee kuweka simulizi hizi kila siku unaweza kutununulia kikombe cha kahawa kama mchango wako kuanzia Tsh 1000 au zaidi kupitia Airtel Money – 0686638386 – MUSA MWAKISASA

What do you think?

1.2k Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Binance Affiliate Program (Join And Increase Your Revenue)

Adekunle Gold – It Is What It Is (Music & Lyrics)