Penzi Bila Maumivu (Sehemu ya 3)

Maisha yaliendelea zaidi. Mwaka wa tatu ulipoingia baada ya kuishi maisha ya ndoa na mkewe, wakapata wageni Wazungu kutoka nchini Uingereza ambao walifika hapo kwa ajili ya kueneza elimu ya ufugaji katika vijiji mbalimbali.
Miongoni mwa Wazungu hao wanne waliofika kijijini hapo alikuwepo msichana mrembo aliyeitwa kwa jina la Tatiana.

Wazungu hao walikuwa msaada mkubwa, hawakuwa na maisha ya kifahari kijijini hapo, walisaidiana na wanakijiji wengine kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo.
Tatiana ambaye alionekana kuwa mrembo zaidi, kila siku akawa akiamka asubuhi na kuwakusanya watoto wengi na kuanza kucheza nao. Maisha ya kijijini yakawa tofauti, amani ikatawala, watu wengi wakawapenda Wazungu hao walioonekana kuleta mabadiliko makubwa.
“Ni msichana mrembo, anavutia machoni kwa kila mwanaume,” alisema jamaa mmoja, aliyagandisha macho yake usoni mwa Tatiana aliyekuwa akicheza na watoto.
“Kwa mfano ukawa na msichana kama huyu, yaani kwa mfano tu, halafu akakupenda, hivi si itakuwa balaa kijijini!” alisema jamaa mwingine.

“Ndiyo hivyo! Anavutia sana jamani.”
Tatiana akawa stori ya kijijini hapo, watu waliendelea kumpenda sana. Mpaka mwezi wa sita unaingia baada ya kukaa kijijini hapo, Wazungu wale wakaamua kuondoka kurudi nchini Uingereza kitu kilicholeta majonzi makubwa.
Mwaka uliofuata, Mwiku akapata watoto wawili, walikuwa mapacha, aliwapenda mno, aliwajali na mapenzi zaidi yakawa kwa mkewe. Hiyo ndiyo ilikuwa familia yake, alipata watoto watatu kwa mke wake, hakutaka tena kuwa na mtoto mwingine, alimshauri mkewe kukubaliana naye, wote wakakubaliana hao ndiyo wangekuwa watoto wa mwisho.
Maisha yalibadilika, baada ya mzee Mwiku kufariki, akaamua urithi wake wote auache kwa mtoto wake, Frida ambaye hakuwa mbinafsi, akawagawana na watoto wengine, kila mmoja akaondoka zake, waliotaka kuuza, waliuliza na waliotaka kuziendeleza mali hizo wakiwemo ng’ombe, walifanya hivyo.

Baada ya mwaka kupita, Sangiwa akashauri wahame hapo na kuhamia katika Kijiji cha Chibe alipozaliwa, Frida hakuwa na kipingamizi, wakahamia huko.
Kila mtu aliyemuona Sangiwa alishangaa, walimfahamu sana, alikuwa kijana masikini ambaye aliondoka kijijini hapo, sasa ilikuwaje awe na mali nyingi, tajiri kiasi hicho?
Alipoingia hapo Chibe tu, kitu cha kwanza ni kujenga nyumba ya kisasa, iliyojengwa kwa matofali na kuezekwa mabati. Kila mwanakijiji akamuheshimu kijana huyo aliyekuwa masikini wa kutupwa kipindi cha nyuma.
“Mume wangu,” aliita Frida.
“Unasemaje mke wangu?”
“Nahisi nina mimba.”
“Unasemaje?”
“Nahisi nina mimba,” alisema Frida huku akiwa amelishika tumbo lake, Sangiwa akachanganyikiwa kwani hakutegemea kupata mtoto mwingie.
“Hebu nione tumbo.”
Akaligusa tumbo la mke wake, Frida.
“Mh!” alijikuta akiguna.

Wote wawili hawakutaka kuwa na mtoto, tayari Frida alikuwa mjauzito kitu kilichomkasirisha kila mmoja. Hawakuwa na jinsi, kile walichokuwa hawakitaki kilikwishatokea hivyo walitakiwa kukubaliana na ukweli wenyewe.
Sangiwa akamuahidi mke wake kwamba angekuwa naye bega kwa bega kuhakikisha mimba inakuwa salama na mwisho wa siku kujifungua mtoto mzuri aliye na afya bora kama alivyofanya vipindi vyote ambavyo Frida alikuwa mjauzito.
Siku zikaendelea kukatika, miezi ikasonga mbele na hatimaye baada ya miezi tisa kukamilika, watu wakajikusanya nje ya nyumba yake kwa ajili ya kusikia ni mtoto wa jinsia gani ambaye angezaliwa siku hiyo.

Kila mtu aliyekuwa mahali hapo alionekana kuwa na furaha, roho nzuri aliyokuwa nayo Sangiwa iliwafanya watu wengi kumpenda na kumtakia mafanikio katika maisha yake yote.
“Natumaini Mungu atakuwa pamoja na mkeo,” alisema mwanaume mmoja, alikuwa akimwambia Sangiwa.
“Natumaini hilo, nina furaha ya ajabu, hatimaye mtoto wangu wa nne anazaliwa,” alisema Sangiwa huku akichia tabasamu pana.
Dakika ziliendelea kusonga mbele, baada ya dakika hamsini, mwanamke mmoja akatoka ndani ya chumba kile, alionekana kuwa na furaha mno huku akiwa na presha kubwa.

Mwanamke yule akaanza kutembea kwa mwendo wa harakaharaka kuelekea kule alipokuwa Sangiwa na wanaume wengine, alikuwa na taarifa nzuri ya kumpa Sangiwa juu ya kile kilichokuwa kimeendelea mule ndani.
“Kuna nini?” aliuliza Sangiwa.
“Hongera sana.”
“Mtoto gani?”
“Wa kike.”
“Unasema kweli?”
“Ndiyo! Ni mzuri kama mama yake,” alisema mwanamke yule.
Sangiwa hakutaka kubaki hapo, alichokifanya ni kusimama na kuanza kuelekea kule ilipokuwa nyumba yake. Kwa kumwangalia tu, wala isingekupa wakati mgumu kugundua alikuwa na furaha mno.

Alipoifikia nyumba ile, akaufungua mlango na kuingia ndani. Alichokiona ndicho alichoambiwa, mke wake, Frida alikuwa hoi, wanawake waliochukua nafasi za manesi, wakunga walikuwa pembeni yake huku mmoja wao akiwa amembeba mtoto huyo aliyekuwa akilia mfululizo.
Akaanza kupiga hatua mpaka pale aliokuwepo mke wake na kuushika mkono wake. Frida alipomuona mume wake tu, akaachia tabasamu pana.
“Hongera sana mke wangu,” alisema Sangiwa.”
“Nashukuru sana.”
“Unamkumbuka Tatiana?”
“Ndiyo!”
“Naomba tumpe jina hilo kama ukumbusho wa Mzungu yule,” alisema Sangiwa.
“Hakuna tatizo.”

Tatiana alikuwa msichana mzuri, uzuri aliourithi kutoka kwa mama yake. Alivutia kwa kila mwanaume aliyekuwa akimwangalia kiasi cha wengi kusema angewa miongoni mwa wasichana ambao wangekuja kutikisa sana katika Kijiji cha Chibe na vijiji vingine pia.
Alichukua kila kitu kutoka kwa mama yake, kwa kumwangalia, kwa mbali Tatiana alionekana kuwa na mchanganyiko wa rangi, alipendwa na kila mtu huku watu wengine wakitaka kumbeba, mikono yao kuwa na mtoto kama Tatiana ilikuwa ni faraja kubwa.
Frida alimlea mtoto wake kwa mapenzi ya dhati, alikuwa akimbembeleza kila alipokuwa akilia huku kila siku akimnyonyesha kitu kilichomfanya kuwa na afya njema kabisa.
Wakati mwezi wa sita unakatika, Frida akahisi kwamba mtoto wake alikuwa na tatizo kwani kila alipokuwa akiuchezesha mkono wake mbele ya uso wa Tatiana kwenda huku na kule, mboni za Tatiana wala hazikucheza.
“Mh!” aliguna Frida.

Hali hiyo ilimshangaza, haikuwa kawaida kwani alikuwa na watoto, tangu walipokuwa na muda huo, kila alipokuwa akiuchezesha mkono wake, zile mboni nyeusi zilikuwa zikihama kwenda huku na kule kuufuata mkono ule.
“Huyu mtoto ana nini?” aliuliza Frida.
“Kwa nini?”
“Mboni zake hazichezi kabisa.”
“Unasemaje?”
“Ndiyo hivyo! Hebu jaribu kuchezesha vidole vyako mbele yake,” alisema Frida, alikuwa akimwambia mumewe, Sangiwa ambaye akafanya hivyo, kweli mboni hazikuwa zikicheza.
Hilo likaonekana tatizo kubwa, wazazi hao wakachanganyikiwa, wakajua kulikuwa na kitu hakikuwa sawa kabisa, walichokifanya ni kusafiri mpaka Shinyanga mjini ambapo huko wakampeleka katika hospitali ya mkoa ambapo madaktari wakaanza kumpima na kugundua tatizo.
“Poleni sana,” alisema daktari kwa sauti ya taratibu.
“Kuna nini? Mbona pole tena?”
“Mtoto wenu ni mzuri ila ni kipofu.”
“Unasemaje?”
“Tatiana ni kipovu, ana upofu wa kuzaliwa,” alijibu daktari yule.
Frida akashindwa kujizuia, majibu ya daktari yule yalimfanya kuhuzunika na baada ya sekunde chache tu, akaanza kulia kama mtoto huku akimlaumu Mungu kwa kile kilichotokea.
Mume wake, Sangiwa akashindwa kumfariji kwani hata na yeye alikuwa akibubujikwa na machozi tu, moyo wake ulimuuma pia mpaka kufikia kipindi akahisi hasira zake zikipanda dhidi ya Mungu.

Moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali, hakuamini kama mtoto wake wa mwisho ambapo baada ya hapo angejizuia kuzaa tena alikuwa kipofu, kila alipomwangalia, moyo wake uliendelea kumuuma mno.
Hawakuwa na jinsi, wakarudi kijijini huku wakiwa na huzuni tele. Hawakutaka kuficha chochote kile, wakawaambia wanakijiji wengine ambao walizipokea taarifa hizo wakiwa na majonzi tele.
“Poleni sana.”
“Asanteni, haina jinsi, kila kitu ni mipango ya Mungu,” alisema Frida huku akiendelea kububujikwa na machozi.

Huo ndiyo uliuwa mwanzo wa kila kitu. Mtoto Tatiana akaanza kukua, alipofikisha mwaka mmoja, akaanza kujifunza kutembea. Hapo ndipo Frida alipoumia zaidi, kila alipomwangalia mtoto wake, alikuwa akipapasa kila alipokwenda, hakuona, aliishi kwa hisia, kuna wakati alikuwa akijikwaa na kudondoka, alisimama na kuendelea tena.
Si Frida tu aliyemuonea huruma Tatiana bali hata wanakijiji wengine. Miaka ikakatika zaidi, uzuri wake ukaanza kujidhihirisha mbele ya watu wengine, baada ya miaka kumi, Tatiana akawa msichana mrembo, alikuwa akisoma lakini vitabu vyake vyote vikiwa na alama za nukta tu.
Hakuona kitu chochote kile, alinyimwa uwezo wa kuona lakini darasani, Tatiana alikuwa mwanafunzi mwingine kabisa. Uwezo wake mkubwa ukamshangaza kila mtu. Wengi walisema alikuwa genius kwani hata kama hakuwepo shuleni, kile walichofundishwa wanafunzi wengine kilipotoka katika mitihani, alifanya vizuri na kuongoza.

Baada ya kufikisha miaka kumi na tano, Tatiana akamaliza kidato cha nne. Urembo wake, ukaendelea kuwapagawisha wavulana wengi kijijini pale. Alikuwa mkimya, kila alipokaa, pembeni kulikuwa na fimbo yake ambayo ilimuongoza kutembea kila alipotaka kwenda.
“Mama…” aliita Tatiana.
“Unasemaje binti yangu?”
“Hivi kuna siku nitaweza kuona?”
“Mh! Kwa kweli sifahamu.”
“Natamani nione, najiona kutokukamilika pasipo kukuona mama yangu kipenzi, ninapenda nione kama wengine mama,” alisema Tatiana huku machozi yakianza kumbubujika.
Frida akashindwa kujizuia, maneno aliyoyazungumza binti yake yaliuchoma moyo wake vilivyo. Ni kweli alijua binti yake alikuwa na kiu ya kutaka kuona tena lakini hakuwa na jinsi, alizaliwa akiwa hivyo, walimpeleka katika hospitali nyingi lakini huko kote walisema kama alizaliwa hivyo, asingeweza kuona tena.

Mbali na kuwa kipofu, Mungu alimpa uzuri wa sura na umbo, wanaume wengi waliokuwa wakimwangalia, walimmezea mate lakini msichana huyo hakutaka kukubaliana na mtu yeyote, hakuamini kama hapa duniani kungekuwa na mwanaume ambaye angependa kuwa na mke kipofu.
Uzuri wake wa sura aliokuwa amepewa, haukuwa peke yake bali Tatiana alipewa na uwezo mkubwa wa kuimba. Alikuwa na sauti nzuri, kanisani, alikuwa mwanakwaya, tena yule aliyewaongoza wote.
Alipokuwa akiimba, kila aliyeisikia sauti yake, alikiri hakuwahi kumuona msichana aliyekuwa akiimba kwa sauti nzuri kama Tatiana. Kanisa lilipokuwa likiandaa mikutano kijijijini hapo au hata kwenye vijiji vya jirani, Tatiana ndiye alikuwa muimbaji kiongozi, sauti yake, ilizitetemesha ngoma za masikio ya watu wengi.

Je, nini kitaendelea?


Asante kwa muda wako kusoma kwenye blog hii, natumaini umefarijika vya kutosha. Kutuunga mkono ili tuendelee kuweka simulizi hizi kila siku unaweza kutununulia kikombe cha kahawa kama mchango wako kuanzia Tsh 1000 au zaidi kupitia Airtel Money – 0686638386 – MUSA MWAKISASA

What do you think?

538 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

The 20 Richest Comic Book Characters of All Time

Careerfy 6.1.0 – Job Board WordPress Theme